National News
Mahakama ya Shanzu Yamtaka ODDP Kuwasilisha Mashtaka Mapya Dhidi ya Wakurugenzi Wawili
Mahakama ya Shanzu mjini Mombasa imemtaka Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini ODPP Renson Ingonga kuwasilisha mashtaka sahihi dhidi ya wakurugenzi wakuu wawili wa chuo kikuu cha North Western Christian waliokamatwa.
Hakimu wa Mahakama hiyo ya Shanzu Leah Juma amepinga mashtaka 120 yaliowasilishwa mbele yake na Ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma dhidi ya washukiwa hao akiwemo Moses Masiga na Jackson Khayumba.
Kulingana na hati kiapo kilichowasilishwa Mahakamani dhidi ya wawili hao, kimeeleza kwamba Masiga na Khayumba wanatuhumiwa kwa kosa la kuendesha chuo ambacho bila kukisajili rasmi kwa Tume ya elimu ya vyuo vikuu nchini.
Katika maelezo zaidi yaliowasilishwa Mahakamani, ni kwamba mnamo Oktoba 13 mwaka 2020 katika mataa wa Bombolulu eneo bunge la Nyali kaunti ya Mombasa wawili hao na wengine ambao hawakuwa mahakamani, walishirikiana kuanzisha chuo hicho bila ya kuzingatia sheria.
Wawili hao pia wanatuhumiwa kutoa vyeti vya kuhitimu kwa mahafali bila ya chuo hicho kusajiliwa, kosa wanalodaiwa kulitekeleza mnamo mwezi Februari 28 mwaka huu katika maeneo ya Nyali kaunti ya Mombasa.
Hata hivyo, wawili hao hawakusomewa mashtaka huku Hakimu mkuu Leah Juma akisema nakala ya mashtaka ilikuwa na kasoro nyingi na kuwaachilia wawaili hao kwa dhamana ya shilingi nusu milioni au pesa taslimu shilingi laki 4 kila mmoja na kesi hiyo ikapangwa kutajwa mnamo tarehe 7 mwezi Aprili mwaka huu.