News

Wavuvi wawili wafa maji Watamu,Kilifi

Published

on

Jamii ya wavuvi katika eneo la Watamu eneo bunge la Kilifi Kaskazini inaiomba serikali ya kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa kununua boti za uokozi ili kusaidia kuokoa maisha wakati kunapotokea dharura baharini.

Hii ni baada ya wavuvi wawili kupotoea katika bahari hindi eneo la Watamu walipokuwa wakiendeleza shughuli zao za uvuvi siku ya Alhamisi 24, Julai 2025.

Kufikia sasa wawili hao hawajapatikana licha ya juhudi za wadau mbalimbali ikiwemo jeshi la wanamaji kuwatafuta.

Kiongozi wa vijana eneo la Watamu Bakari Shaban, alisema kuwa juhudi za kuwatafuta wavuvi hao ambao ni mandugu wanaotambulika kama Athman Lali na Huzefa Lali zinaendelea.

Shaban alisistiza haja ya serikali kuangazia suala la ununuzi wa mashua za kisasa za uokozi ili kupunguza visa vya wavuvi kuangamia baharini wakati wanapoelekea kuvua.

“Mpaka sasa juhudi zote zimefanyika lakini ndugu zetu hatujajua wako sehemu gani, serikali itusaidie mji wetu wa Watamu ni mji wa utalii, tunaomba tupate boti za kuokoa maisha baharini, popote alipo waziri Ali Joho angalau tupate boti za uokozi kama mbili hapa Watamu ni kitovu cha utalii kunamahoteli mengi, watalii wote wanaokuja Watamu mpaka leo hakuna boti za uokozi”, alisema Shaban.

Kwa upande wao wazazi wa wavuvi waliopotea baharini Lali Athman Lali na Dhurai Mohamed Ali waliiomba serikali kuweka juhudi zaidi za kuwasaidia kuwapata wana wao kwani ndio tegemeo kubwa kwa familia yao.

“Uko usaidizi unatumika, kuna vijana wanaojitolea kwa maboti wanaenda ile sehemu ambayo wavuvi wanavua, wanajaribu kuzunguka lakini toka siku hiyo hawajapata chochote: Katika Maisha yangu mimi nawategemea hawa watoto kunisomeshea hawa watoto wangu ambao ni wadogo zao mashule, kwa chakula kwa hivyo naomba serikali inisaidie kwa sababu ndio tegemeo langu hao watoto”.walisema wazazi.

Kisa hiki kinajiri miezi kadhaa baada ya mvuvi mmoja kutoka eneo la Mnarani mjini Kilifi kufariki baharini baada ya kugongwa kichwani kwa pondo na wavuvi wenzake kulipotokea mzozo kuhusu pato la samaki.

Kufikia sasa mwili wa mvuvi huyo haujapatikana

Taarifa ya Mwanahabari wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version