Sports
Klabu ya KCB yatwaa ubingwa wa Raga ya Driftwood 7s mjini Mombasa
Klabu ya KCB ndiyo mabingwa wa michuano ya Raga ya wachezaji saba kila upande ya Driftwood 7s iliyofanyika mjini Mombasa.
Hii ni baada ya kuibuka na ushindi wa alama 15–14 dhidi ya klabu ya Strathmore Leos katika fainali ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mombasa Sports Club.
KCB, maarufu kama Mabenki, walianza mchezo kwa kasi na kutawala kipindi cha kwanza. Hata hivyo, Strathmore walirejea kwa nguvu kipindi cha pili na walikuwa karibu kusawazisha, lakini walikosa kwa pointi moja pekee.
Katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu, Kabras RFC waliibuka na ushindi wa alama 21–10 dhidi ya Nakuru RFC, na hivyo kupanda kutoka nafasi ya nne waliyoshikilia mwaka 2024.
Wakati huo huo, katika Divisheni ya Pili, Zetech Oaks waliibuka kidedea kwa kuichapa NYS Spades kwa alama 10–0, na kutwaa ubingwa bila kuruhusu bao lolote.