News
UN yakosoa mauaji ya Saba saba
Ofisi ya kamishna mkuu wa haki za kibinadamu wa umoja wa mataifa (OHCHR) imeibua wasiwasi kuhusu maandamano ya siku ya Saba Saba nchini Kenya, ambapo makumi ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.
Katika taarifa yake siku ya Jumanne, kamishna mkuu wa umoja wa mataifa wa haki za kibinadamu Volker Türk alilaani ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Kenya, na kuahidi kushirikiana na Kenya katika kutatua changamoto vile vile katika uchunguzi.
“Tumesikitishwa sana na mauaji ya jana ya takriban watu 10, pamoja na uporaji na uharibifu wa mali nchini Kenya wakati polisi na vikosi vingine vya usalama vilijibu maandamano ya ghasia katika mji mkuu wa Nairobi na kaunti zingine 16. Risasi za sumu, risasi za mpira, gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha zilitumika,” ilisema OHCHR kupitia msemaji wake Ravina Shamdasani.
Türk alitoa wito wa utulivu pamona na heshima kamili kwa uhuru wa kujieleza, kujumuika na kukusanyika kwa amani.
“Ni muhimu kwamba malalamiko halali katika mzizi wa maandamano haya yashughulikiwe,” alisema.
Kamishna Mkuu pia alihimiza kwamba mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu “kuchunguzwa kwa haraka, kikamilifu, kwa uhuru na kwa uwazi.”
Wakati wa maandamano ya Julai 7, 2025, polisi waliripoti kwamba raia 11 waliuawa na 567 walikamatwa.
Pia, huduma ya kitaifa ya polisi (NPS) ilisema maafisa 52 na raia 11 walijeruhiwa, magari 12 ya polisi, magari 3 ya serikali na magari 4 ya raia yaliharibiwa.
“Chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, nguvu ya kimakusudi ya maafisa wa kutekeleza sheria, ikiwa ni pamoja na silaha, inapaswa kutumika tu inapobidi ili kulinda maisha kutokana na tishio linalokaribia,” aliongeza Türk.
Maandamano yaliyoshuhudiwa siku ya Saba Saba yalikuja baada ya wiki mbili tu baada ya raia 15 kuuawa mnamo Juni 25, 2025.
Kisha, wakenya waliandamana katika ukumbusho wa mauaji ya zaidi ya watu 60 wakati wa maandamano ya kupinga ushuru mnamo Juni 2024.
Taarifa ya Joseph Jira