Business
Wakaazi wahofia mkurupuko wa magonjwa baada ya kuuziwa nyama Malindi
Wakaazi wa mji wa Malindi kaunti ya Kilifi wanaishi kwa hofu ya mkurupuko wa magonjwa baada ya kulalamikia kuuziwa nyama ya mifugo ambayo haijakaguliwa na maafisa wa mifugo eneo hilo.
Wakielezea manung’uniko yao, wakaazi hao walioongozwa na Kensa Ondiek walisema nyama ya mifugo inayouzwa eneo hilo haijakaguliwa, akiongeza kwamba kichinjio cha kipekee mjini humo pia kina wafanyikazi ambao ni wa umri wa chini ya miaka kumi na nane.
Wakaazi hao pia walisema mazingira ya kufanya kazi katika kichinjio hicho nai ya kutatanisha huku wachuuzi wa nyama wakifanya biashara zao mahali peupe na pachafu.
Vyombo vya Habari vilidhibitisha matukio hayo kupitia picha za watoto wakifanya kazi katika kichinjio hicho na kuchinjwa kwa mifugo siku ya Jumapili.
Afisa wa mifugo eneo la Malindi Godreck Mwaringa alitetea madai hayo akisema kwamba mifugo inayochinjwa katika kichinjio hicho hukaguliwa pindi inapofika, kabla na baada ya kuchinjwa.
Aliongezea kwamba maafisa husika hufanya kazi kuanzia siku ya Jumatatu hadi Jumamosi, japo akaweka wazi kwamba huenda wanaochinjwa siku ya Jumapili huwa ni uchinjaji wa dharura ambao pia nyama yake inafaa kukaguliwa kabla ya kuuzwa.
Hata hivyo alitoa tahadhari kwa wakazi wa Malindi kuhakikisha wananunua nyama iliyokaguliwa huku akionya kuwa watakaopatikana na mifugo wala nyama ambayo hazijakaguliwa watashtakiwa.
Taarifa ya Eric Ponda