News
Kampuni ya Simba Cement yafungwa, Kaloleni
Serikali ya kaunti ya Kilifi kwa ushirikiano na Wizara ya Madini imesitisha rasmi shughuli zote za uchimbaji madini zinazotekelezwa na kampuni ya Simba Cement eneo la Kaloleni kaunti ya Kilifi.
Agizo hilo limetolewa na Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro pamoja na Waziri wa madini na raslimali za uchumi wa bahari nchini Ali Hassan Joho, wakisema kampuni hiyo imeshindwa kufuata sheria za mazingira na haiwafaidi wakaazi wa eneo hilo.
Viongozi hao walisema shughuli za uchimbaji wa kampuni hiyo zimekuwa zikiathiri mazingira na wakazi wa maeneo ya karibu, huku wakiahidi kwamba serikali haitavumilia ukosefu wa uwajibikaji unaotishia afya na maisha ya wananchi.
Walisisitiza kwamba kampuni hiyo haitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake hadi pale itakapokidhi masharti yote ya kisheria na kuthibitisha kwamba haileti madhara kwa binadamu wala mazingira.
“Hii kampuni wacha nikuambie waziri haisadii wananchi wa Kilifi kwa chochote waziri, na leo hii watu wa kambe ribe mnisikize na mnisikize kwa makini, vile nilifanya Jaribuni ndivyo nitakavyofanya leo, kuanzia kesho asubuhi na nitawafuata na barua kesho mwelezeni mwajiri wenu kwamba hii kampuni tumeifunga na nitawafuata na barua”, alisema Gavana Mung’aro.
Hatua hii iliungwa mkono na baadhi ya viongozi wa jamii na wanaharakati wa mazingira, wakisema kuwa ni wakati wa kuwajibisha wawekezaji wanaokiuka haki za wananchi kwa msingi ya maendeleo.
Simba Cement, ambayo imekuwa ikihusishwa na miradi mikubwa ya ujenzi, sasa inalazimika kukabiliwa na masharti mapya kabla ya kurejelea shughuli zake za kawaida.
Taarifa ya Elizabeth Mwende