News

Watoto wa umri wa miaka 14 na 16 watoa ushahidi dhidi ya Mackenzie

Published

on

Mashahidi wawili wa umri mdogo wameelezea Mahakama ya Mombasa ukatili waliopitia mikononi mwa wazazi wao kufuata maagizo ya mchungaji Paul Mackenzie katika kesi ya mauaji inayomkabili pamoja na washukiwa wengine 94.

Mtoto wa kwanza mwenye umri wa miaka 16 alisimulia jinsi mamake alivyomuondoa shuleni baada ya kufuata mafundisho ya Mackenzie kupitia runinga, kuuza mali ya nyumbani ili kufadhili safari yao hadi msitu wa Shakahola.

Aidha alieleza Mahakama kwamba wakiwa njiani walifungiwa kwenye hema na kulazimishwa kufunga kwa imani ya kuharakisha safari ya kwenda mbinguni na pia jinsi alivyoadhibiwa vikali kwa kuiba chakula kutokana na njaa na hatimaye kutoroka kwa msaada wa wazee wa kijiji.

Shahidi wa pili, ambaye ni mtoto wa miaka 14, alielezea Mahakama jinsi walivyonyimwa haki ya kwenda shule kwa madai kuwa elimu ni ya kishetani, akieleza kwamba waliwekewa vizuizi vya kutoka nje huku Chifu wa eneo hilo akifanya ukaguzi wa wanafunzi.

Mashahidi hao pi walielezea ibada, mikutano ya maombi na kufunga kwa lazima chini ya uongozi wa Mackenzie, ambapo mazishi yalijulikana kama “harusi.”

Kesi hiyo itaendelea lhuku mashahidi zaidi wakitarajiwa kufika Mahakamani mbele ya Hakimu mkuu Alex Ithuku.

Taarifa ya Mwanahabari wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version