News
Mahakama kuu yabatilisha uamuzi wa bunge la Kilifi dhidi ya Spika Mwambire
Mahakama kuu ya Malindi imebatilisha uamuzi wa bunge la kaunti ya Kilifi wa kumtimua Mamlakani Spika wa bunge hilo Teddy Mwambire na kuagiza Spika Mwambire kurejea kazini.
Jaji Njagi aliagiza pia Spika Mwambire kurejea kazi licha ya bunge hilo kumtimua Mamlakani Juni 30 kutokana na madai ya kutokuwa na imani naye.
Jaji Njagi alilitaka bunge hilo kuzingatia kanuni na sheria na kumpa nafasi Spika Mwambire kutekeleza majukumu yake ya kikazi kwa mujibu wa sheria hadi kesi hiyo iliyowasilishwa na Mahakamani itakaposkizwa na kuamuliwa.
Jaji huyo hata hivyo aliwasilisha faili ya kesi hiyo kwa Jaji Mugure Thande ambapo kesi hiyo itaskizwa rasmi mnamo tarehe 14, Julai mwaka huu huku walalamishi wa kesi hiyo akiwemo Kassim Mwadena na Emmanuel Kazungu Chai wakidai kwamba bunge hilo lilikiuka sheria na haki za Spika Mwambire.
Itakumbukwa kwamba mnamo Juni 30 mwaka huu, bunge la kaunti ya Kilifi lilipiga kura 40 kati ya 50 na kuidhinishwa kutimuliwa Mamlakani kwa Spika Mwambire kwa misingi ya ukiukaji wa Katibu, utumizi mbaya wa ofisi ya umma, ukandamizaji wa miradi ya serikali ya kaunti ya Kilifi miongoni mwa shtuma zengine.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi