News
IEBC yahakikishia wakenya usalama wa taarifa za usajali
Tume uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) imerejesha tovuti yake ambayo wapigakura huthibitisha taarifa zao za usajili, baada ya kipindi cha ukarabati.
Hii ni kufuatia malalamishi ya umma kuhusu hitilafu isiyoeleweka ambayo ilisababisha mamilioni ya wakenya kushindwa kupata taarifa zao za usajili kama wapigakura.
Tume hiyo ilitangaza kwamba tovuti hiyo sasa imerejea mtandaoni, kufuatia kipindi cha ukarabati wa mfumo unaolenga kuhamisha miundombinu yake ili kuimarisha utendakazi na usalama.
Tangazo hilo lilifuatia siku za sintofahamu ambapo wakenya hawakuweza kuthibitisha maelezo yao ya usajili, iwe kupitia tovuti ya IEBC au kwa njia ya ujumbe mfupi.
Wapigakura walipata ugumu wa kutuma nambari ya kitambulisho au ya pasipoti pamoja na mwaka wao wa kuzaliwa, kulingana na mahitaji ya IEBC.
Njia zote mbili za uthibitishaji hazikuweza kufikiwa wakati wa ukarabati, na hivyo kusababisha wasiwasi kuongezeka, haswa wakati joto la kisiasa linapozidi kuongezeka kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumapili 6, Julai 2025 bodi ya uchaguzi iliwahakikishia wapiga kura, ikisema, “Tungependa kuwahakikishia wakenya wote kwamba maelezo ya usajili wa wapigakura 22,120,458 waliojiandikisha, kama yalivyorekodiwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022, yanasalia shwari na salama.
IEBC iliongeza kuwa uboreshaji wa mfumo ulikuwa muhimu ili kuimarisha utoaji wa huduma kupitia utendakazi bora wa mfumo na usalama wa data.
Taarifa ya Joseph Jira