News
Philip Charo ateuliwa kaimu waziri wa barabara Kilifi
Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro amefanya mabadiliko katika serikali yake na kumteua afisa mkuu mtendaji wa idara ya barabara Philip Charo kuwa kaimu waziri katika idara ya barabara.
Hii ni baada ya kuchaguliwa kwa aliyekuwa waziri wa idara hiyo Catherine Kenga kuwa spika wa bunge la kaunti ya Kilifi.
Katika taarifa kupitia msemaji wa kaunti Johnathan Mativo, afisa mkuu mtendaji wa idara ya maswala ya fedha Hezekiah Mwaruwa pia aliteuliwa kuwa afisa mkuu mtendaji katika ofisi ya gavana.
Mativo alisema kwamba mabadiliko hayo yanaanza kutekelezwa mara moja ingawa ni ya mda.
Catherine Kenga alijiunga na utumishi wa serikali ya kaunti ya Kilifi mnamo mwaka 2023 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 uliopelekea kuchaguliwa kwa gavana Gideon Maitha Mung’aro.
Pia amewahi kuhuduma kama kaimu katibu wa kaunti baada ya kutimuliwa kwa Martin Mwaro.
Catherine Kenga alichaguliwa kuwa spika wa bunge la kaunti ya Kilifi katika kikao maalum ambacho kiliandaliwa katika bunge hilo Jumatu Julai 21 2025.
Kenga anachukua hatamu ya kuliongoza bunge hilo kutoka kwa aliyekuwa spika Teddy Mwambire ambaye alitimuliwa mapema mwezi uliopita Juni 30, 2025 kupitia kura ya maoni.
Mwambire alibanduliwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa katiba.
Taarifa ya Joseph Jira