News
Thaura Mweni:Spika anafaa kufahamu utendakazi wa Bunge
Mwakilishi wadi wa Sokoke kaunti ya Kilifi Thaura Mweni ametaja zoezi la kumchagua spika mpya wa bunge la kaunti ya Kilifi linalofanyika hii leo kama litakaloendeshwa kwa njia huru na wazi.
Katika mahojiano na Coco Fm, Thaura alipinga madai kuwa huenda kuna baadhi ya wawakilishi wadi ambao walipewa hela ili kumuunga mkono mgombea fulani wa wadhfa huo.
Thaura alisema wanatarajia mgombea atakayechaguliwa kufahamu kwa undani mahitaji ya wakaazi wa kaunti ya Kilifi, vile vile kuzingatia utendakazi wa bunge hilo kwa ushirikiano na wadau wengine.
“Kwanza ni mtu ambaye anajua wananchi wa Kilifi wanahitaji nini kwa sababu bunge la Kilifi linafaa kujitegemea zaidi, lakini pia liweze kufanya kazi na wadau wengine, kwa hivyo ni mtu mwenye ugahamu wa serikali jinsi ambavyo zinafaa kufanya kazi”, alisema Thaura.
Zoezi hilo linafanyika baada ya Teddy Mwambire kubanduliwa uongozi na wawakilishi wadi Juni 30, 2025, kupitia kura ya maoni, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa katiba.
Shughuli hiyo inafanyika licha ya mahakama nchini kumwagiza Mwambire kuendelea kushikilia wadha huo.
Miongoni mwa wanaowania wadhifa huo ni pamoja na wakili Faith Zawadi Kingi, Tendai Mtana Lewa, Catherine Kenga, na Mazera Shadrack.
Taarifa ya Joseph Jira