News

11 wazuiliwa rumande Malindi kwa madai ya Uhalifu na ugaidi

Published

on

Mahakama mjini Malindi kaunti ya Kilifi iliwaamuru washukiwa 11 waliokamatwa katika kijiji cha Kwa Binzaro kilomita sita kutoka eneo la Shakahola kuzuiliwa rumande kwa mda wa siku 30 ili kuruhusu uchunguzi zaidi.

11 hao walikamatwa baada ya kuhusishwa na madai ya uhalifu, ugaidi na kwenda msituni na watoto.

Awali polisi ilitangaza kupata mwili mmoja na mafuvu mawili ya binadam kwenye nyumba moja katika kijiji hicho.

Kulingana na polisi watu wanne waliokolewa katika oparesheni hiyo.

Kamishna wa kaunti ya Kilifi Josephat Biwot alisema oparesheni hiyo iliyohusisha wakaazi, watu watatu kati ya wanne waliookolewa walionekana wakiwa dhaifu kuliko hali yao ya kawaida.

Biwot alidokeza kuwa wahusika hawakupatikana nyumbani wakati wa oparesheni hiyo na haikubainika kilichokuwa kikiendelea.

Eneo la Shakahola kaunti ya Kilifi liligonga vichwa vya habari baada ya kugunduliwa makaburi ya halaiki yaliyomhusisha mhubiri tata Paul Mackenzi ambaye kwa sasa anaendelea kuzuiliwa rumande pamoja na washirika wake wakati kesi ikiendelea.

Mwili na mafuvu hayo yalipelekwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version