News
Catherine Kenga ndiye spika mpya wa bunge kaunti ya Kilifi
Catherine Kenga amechaguliwa kuwa spika wa bunge la kaunti ya Kilifi katika kikao maalum ambacho kiliandaliwa katika bunge hilo Jumatu Julai 21 2025.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na naibu spika wa bunge hilo Naftal Kombo kwenye majengo ya bunge hilo mjini Malindi, Catherine Kenga alipata jumla ya kura 41, akifuatwa na wakili Faith Zawadi Kingi aliyepata kura 6 huku kura moja ikiharibika.
Wawakilishi wadi watatu walikosa kuhudhuria kikao hicho ingawa sababu za viongozi hao kukosa kuhudhuria hazikuwekwa bayana.
Kenga anachukua hatamu ya kuliongoza bunge hilo kutoka kwa aliyekuwa spika Teddy Mwambire ambaye alitimuliwa mapema mwezi uliopita Juni 30, 2025 kupitia kura ya maoni.
Mwambire alibanduliwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa katiba.
Catherine ni miongoni mwa wagombeaji wanne waliotuma maombi ya kuwania wadhifa huo baada ya kujiuzulu kama waziri wa barabara katika serikali ya Kaunti ya Kilifi chini ya uongozi wa gavana Mung’aro.
Pichani:Kutoka kushoto,Karani wa bunge la kaunti ya Kilifi, Micheal Ngala, gavana Gedion Maitha Mung’aro na spika wa Sasa Catherine Kenga (Picha Kwa hisani
Catherine Kenga atakuwa spika wa tatu kulihudumia bunge hili, baada ya spika wa kwanza Jimmy Kahindi ambaye alihudumu kwa vipindi viwili chini ya uongozi wa gavana Amason Kingi ,ambaye sasa ni spika wa bunge la seneti.
Teddy Mwambire ndio alichukua wadhifa huo baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, aliposhindwa na Kenneth Kazungu Charo almaarufu ‘Tungule’ katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Ganze.
Catherine Kenga sasa anajukumu la kuleta mshikmano katika bunge hilo linalokabiliwa na mgawanyiko kati ya wandani wa gavana Mung’aro kwa upande mmoja na wale ambao walimuunga mkono Teddy Mwambire wakati kura ya kutokuwa na imani naye ilipopigwa.
Kuwepo kwa maafisa wa ngazi za juu kutoka serikali ya gavana Mungaro wakati wa kura hiyo ni ishara ya wazi kwamba spika wa sasa Catherine Kenga ana usuhuba na serikali ya sasa ya gavana Mung’aro.
Hata hivyo, kura hiyo ilipigwa licha ya kuwepo kwa agizo la mahakama lililotolewa wiki mbili zilizopita kusitisha mipango ya kumtimua Teddy Mwambire hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani kusikilizwa na kuamuliwa.
Miongoni mwa walioshiriki kura hiyo ni pamoja na Tendai Mtana Lewa, na Mazera Shadrack.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi