News
Mahamoud Ali Ashinda Uchaguzi wa AUC
Mgombea wa wadhifa ya uwenyekiti wa Tume ya umoja wa Afrika AUC, Mahmoud Ali Youssouf kutoka Djibouti, sasa ndiye Mwenyekiti mpya wa Tume hiyo baada ya kushinda kwa kura 33 katika awamu ya 7.
Hii ni baada ya Raila Odinga kutoka Kenya kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho baada ya kushindwa na Mahmoud katika awamu ya tano na sita katika kinyang’anyiro hicho.
Mahmoud, ambaye katika awamu ya saba amepata kura 33, ambayo ni thuluthi mbili ya kura zote zilizopigwa katika ukumbi wa Nelson Mandela jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, amepewa majukumu yake rasmi.
Wachanganuzi wa maswala ya kisiasa wameipongeza serikali ya Kenya kwa kuonyesha juhudi za kuyashawishi mataifa ya Afrika kumuunga mkono Odinga, japo matokeo hayakuridhisha.
Hata hivyo wanaogombea nafasi hiyo ilikuwa ni pamoja na Raila Odinga wa Kenya, Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar, huku mataifa ya Sudan, Burkina Faso, Mali, Gabon, Niger na Guinea yakifungiwa nje ya uchaguzi huo kutokana na vita katika mataifa hayo.