Entertainment

Kutoka High Heels Hadi Kuimba Peku Stejini, Nyota Ndogo Afunguka

🎙️ “Sauti yangu ndiyo ya kusikiliza – si viatu vyangu.”
Katika dunia ya burudani ambako muonekano hupewa uzito mkubwa, Nyota Ndogo ameamua kuvunja ukimya. Kupitia video yake ya hivi karibuni, msanii huyo maarufu wa Pwani ameweka wazi sababu ya kuimba bila viatu stejini – na jibu lake linauma, linafundisha na linagusa moyo.

Published

on

Katika dunia ya burudani, wasanii hujikuta wakikumbana na mashabiki wa kila aina – wale wanaopenda sana kazi yao, na pia wale wanaouliza maswali au kukosoa kwa mitazamo yao. Hivi karibuni, muimbaji maarufu wa Pwani ya Kenya, Nyota Ndogo, aliamua kujibu swali ambalo limekuwa likizua mjadala mitandaoni: Kwa nini huimbia stejini bila viatu?

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Nyota Ndogo aliweka video akiwa kwenye onyesho la moja kwa moja, akiimba kwa hisia bila viatu. Video hiyo ilisababisha baadhi ya mashabiki kuuliza au hata kukosoa kuhusu muonekano wake huo, jambo lililomchochea kujibu kwa uwazi wa kipekee.

“Wapenzi wangu, nitakuwa najibu lile linalohitaji kujibiwa tu,” Nyota alianza kwa kusema.

Katika maelezo yake ya wazi na yenye kugusa moyo, Nyota Ndogo alisimulia kuwa alipokuwa msichana mdogo anayeanza muziki, alikuwa akivaa viatu vya michuchumio mirefu (high heels) ili aonekane mrefu. Wanaomfahamu vizuri wanajua kuwa urefu wake si mkubwa, na mara nyingi wale wanaomuona kwa mara ya kwanza hushangaa kumwona mfupi kuliko walivyodhani.

Kwa mujibu wake, viatu hivyo virefu viliathiri afya yake ya miguu kwa kiasi kikubwa:

“Miguu yangu ni mikubwa, nilirithi kwa mama. Lakini vile viatu vimeniletea madhara makubwa sana. Sasa ukubwani ndio naona madhara yake. Miguu huuma sana, wakati mwingine hata kutembea huwa shida, hasa mguu wa kushoto ambao huuma kama kidonda.”

Kwa sababu hiyo, amekuwa akilazimika kuvaa viatu vya chini au wakati mwingine kutumbuiza bila viatu kabisa, hasa maumivu yanapokuwa makali sana.

Lakini licha ya hayo, msanii huyo amesisitiza jambo moja muhimu:

“Mkiniona bila (viatu) niacheni tu na musikilize sauti yangu.”

Katika onyesho lake la hivi karibuni lililofanyika mgahawa mmoja Kilifi, ambalo lilikuwa acoustic performance, mashabiki waliweza kushuhudia nguvu ya sauti yake na hisia halisi bila kuangalia muonekano wa nje. Na kama alivyoeleza, onyesho hilo lilikuwa la aina yake:

“It was wow,” alisema Nyota.

Hadithi ya Nyota Ndogo si tu kuhusu muziki au uvaaji wa viatu – ni somo la maisha. Ni ukumbusho kuwa kila msanii ana hadithi ya kipekee nyuma ya pazia. Kabla ya kuhukumu kwa nje, ni vyema kuelewa ndani – na kama alivyoomba, tusikilize sauti yake, si kutazama miguu yake.

Je, umewahi kuhukumiwa kwa muonekano wako bila kueleweka undani wako? Hebu nambie kwenye comment section. 👇

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version