News
NACADA yapendekeza sheria mpya ya kudhibiti pombe
Mamlaka ya kukabiliana na dawa za kulevya na pombe haramu nchini NACADA inaendelea kushikilia pendekezo lake la kutaka umri wa chini wa unywaji wa pombe uwe wa miaka 21.
Mratibu wa Mamlaka hiyo kaunti ya Mombasa, Wangai Gashoka alisema pendekezo hilo limetokana na ongezeko la vijana wadogo wanaotumia pombe kupindukia.
Wangai alisema kuwa utafiti wa NACADA ulionyesha wazi kwamba akili ya binadamu huendelea kukua hadi miaka 25 hivyo mtu akinywa pombe akiwa na umri mdogo huongeza hatari ya uraibu wa mapema.
NACADA sasa inashinikiza pendekezo hilo kufanywa kuwa sheria ambayo itaidhinishwa bungeni na kuanza kutekelezwa kikamilifu.
Ni hatua ambayo ilipigiwa upato na wakereketwa wa kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya akiwemo Famau Mohamed Famau ambaye alisisitiza haja ya mapendekezo hayo kutopuuziwa.
Taarifa ya Hamis Kombe