Entertainment
Kutoka High Heels Hadi Kuimba Peku Stejini, Nyota Ndogo Afunguka
🎙️ “Sauti yangu ndiyo ya kusikiliza – si viatu vyangu.”
Katika dunia ya burudani ambako muonekano hupewa uzito mkubwa, Nyota Ndogo ameamua kuvunja ukimya. Kupitia video yake ya hivi karibuni, msanii huyo maarufu wa Pwani ameweka wazi sababu ya kuimba bila viatu stejini – na jibu lake linauma, linafundisha na linagusa moyo.

Katika dunia ya burudani, wasanii hujikuta wakikumbana na mashabiki wa kila aina – wale wanaopenda sana kazi yao, na pia wale wanaouliza maswali au kukosoa kwa mitazamo yao. Hivi karibuni, muimbaji maarufu wa Pwani ya Kenya, Nyota Ndogo, aliamua kujibu swali ambalo limekuwa likizua mjadala mitandaoni: Kwa nini huimbia stejini bila viatu?
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Nyota Ndogo aliweka video akiwa kwenye onyesho la moja kwa moja, akiimba kwa hisia bila viatu. Video hiyo ilisababisha baadhi ya mashabiki kuuliza au hata kukosoa kuhusu muonekano wake huo, jambo lililomchochea kujibu kwa uwazi wa kipekee.
“Wapenzi wangu, nitakuwa najibu lile linalohitaji kujibiwa tu,” Nyota alianza kwa kusema.
Katika maelezo yake ya wazi na yenye kugusa moyo, Nyota Ndogo alisimulia kuwa alipokuwa msichana mdogo anayeanza muziki, alikuwa akivaa viatu vya michuchumio mirefu (high heels) ili aonekane mrefu. Wanaomfahamu vizuri wanajua kuwa urefu wake si mkubwa, na mara nyingi wale wanaomuona kwa mara ya kwanza hushangaa kumwona mfupi kuliko walivyodhani.
Kwa mujibu wake, viatu hivyo virefu viliathiri afya yake ya miguu kwa kiasi kikubwa:
“Miguu yangu ni mikubwa, nilirithi kwa mama. Lakini vile viatu vimeniletea madhara makubwa sana. Sasa ukubwani ndio naona madhara yake. Miguu huuma sana, wakati mwingine hata kutembea huwa shida, hasa mguu wa kushoto ambao huuma kama kidonda.”
Kwa sababu hiyo, amekuwa akilazimika kuvaa viatu vya chini au wakati mwingine kutumbuiza bila viatu kabisa, hasa maumivu yanapokuwa makali sana.
Lakini licha ya hayo, msanii huyo amesisitiza jambo moja muhimu:
“Mkiniona bila (viatu) niacheni tu na musikilize sauti yangu.”
Katika onyesho lake la hivi karibuni lililofanyika mgahawa mmoja Kilifi, ambalo lilikuwa acoustic performance, mashabiki waliweza kushuhudia nguvu ya sauti yake na hisia halisi bila kuangalia muonekano wa nje. Na kama alivyoeleza, onyesho hilo lilikuwa la aina yake:
“It was wow,” alisema Nyota.
Hadithi ya Nyota Ndogo si tu kuhusu muziki au uvaaji wa viatu – ni somo la maisha. Ni ukumbusho kuwa kila msanii ana hadithi ya kipekee nyuma ya pazia. Kabla ya kuhukumu kwa nje, ni vyema kuelewa ndani – na kama alivyoomba, tusikilize sauti yake, si kutazama miguu yake.
Je, umewahi kuhukumiwa kwa muonekano wako bila kueleweka undani wako? Hebu nambie kwenye comment section. 👇
Entertainment
Joy to The World! Mke wa Michael Yena, Grace Santa, Ajifungua
Mwimbaji wa Injili Michael Yena na mkewe Grace Santa wamebarikiwa na mtoto wao wa kwanza. Jua zaidi kuhusu ujio huu wa neema na wimbo mpya ‘Ametutendea’ unaosindikiza tukio hilo la kipekee!

Ni shangwe! Ni nderemo! Ni vigelegele! Baraka kubwa imetua rasmi kwenye familia changa ya mwimbaji wa nyimbo za Injili, Michael Yena, baada ya mkewe kipenzi Grace Santa kujifungua mtoto wao wa kwanza! 🍼👶
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, Yena alipakia picha na tulipomtafuta mda mchache uliopita akathibitisha habari hiyo njema.
Kwenye Facebook, Yena, aliandika:
“We give God all the Glory. #Ametutendea”
Lakini subiri kidogo! Ikiwa unataka kujua mtoto ni wa kike au wa kiume… tafadhali kaa mkao wa kusubiri 😅. Kulotia maongezi ya njia ya simu, Yena amesema, kwa sasa jinsia ya mtoto itabaki kuwa “fiche”, wakisubiri wakati maalum wa kufanya tangazo rasmi. Hii ni kama suspense ya movie nzuri—yaani hata mtoto wao anaingia duniani na style! 🎬✨
🎶 Wimbo Mpya Wenye Maana Kubwa: “Ametutendea”
Katika kusindikiza ujio wa mtoto wao, Michael Yena ameendelea kusukuma wimbo wake mpya “Ametutendea”—na kwa kweli, jina la wimbo linazungumza moja kwa moja na tukio la maisha yao. Ni ushuhuda wao.
👉 Tazama video ya wimbo huo hapa:
🔗 Ametutendea – Michael Yena (Official Video)
Wimbo huu ni wimbo wa ushuhuda, wa shukrani, na wa imani. Ukiusikiliza huku ukijua kuwa umetoka kwa mtu ambaye ameonja wema wa Mungu kwa kiwango hiki—huwezi kubaki vilevile!
💍 Safari ya Upendo Yao
Kwa wanaofuatilia historia yao ya kimapenzi na kiroho, Michael na Grace walifunga ndoa yao mwezi Aprili mwaka 2024. Kwa kipindi kifupi, wameonyesha mfano wa ndoa yenye msingi wa maombi, heshima na maelewano. Na sasa, wameingia katika ukurasa mpya wa maisha—ukurasa wa uzazi!
Tunawatakia kila la kheri katika safari yao ya kuwa wazazi. Dunia imepata mtoto mwingine wa neema, na hakika tunaamini huyu naye atakuwa baraka kwa vizazi. Kama ilivyo kwa mashairi ya wimbo wao mpya, tunaungana nao kusema kwa nguvu zote:
“AMETUTENDEA!” 🎉
📌 Endelea kutembelea www.cocomedia.co.ke kwa habari za utendeti, matukio ya kusisimua, habari na kila kinachohusu burudani.
Entertainment
Creative Economy Forum 2025: Ruby Kache Uso kwa Uso na Bien
Ruby Kache na Bien wakutana Nairobi kwenye Jukwaa la Uchumi wa Ubunifu! 🌟

Jiji la Nairobi liling’aa zaidi wiki hii baada ya kuandaa Jukwaa la Uchumi wa Ubunifu — tukio la kipekee lililowakutanisha wabunifu, wanamuziki, na wadau wa sanaa kutoka Kenya na Marekani. Mbali na mijadala ya sera na mipango ya maendeleo, tukio hili lilikutanisha watu mashuhuri.
Mrembo wa redio, Ruby Kache, alikutana na nyota wa muziki, Bien aliyekuwa kwenye kundi la maarufu Sauti Sol!
Kwa wanaosikiliza redio, jina la Ruby Kache si geni. Ni mtangazaji machachari wa kipindi cha “The Wave” kupitia Coco FM, kinachoenda hewani kila Jumamosi kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana. Kipindi chake kinajulikana kwa kuangazia maisha ya vijana, muziki wa kisasa, mitindo na mazungumzo yenye msisimko.
Katika kongamano hili, Ruby alihudhuria kama mshiriki, lakini kama ilivyo kawaida yake — aliiba spotlight bila kusema neno jukwaani. Uvaaji wake, tabasamu lake na muingiliano wake na wadau wengine ulitosha kuonyesha uwepo wake wa nguvu.
Moja ya highlights kubwa za siku hii ilikuwa ni wakati Ruby Kache alipokutana na Bien. Ruby alirekodi kipande kifupi na kukipakia kwenye ukurasa wake wa Facebook, huku mashabiki wakishangilia. Bien, nguli wa mziki anayeshikilia tuzo ya muimbaji bora Afrika Mashariki, alikuwa mgeni maarufu katika tukio hilo.
Baadhi ya waunda maudhui maarufu kutoka Pwani waliopamba hafla hiyo ni pamoja na Presenter Kai, Beka Ruga, Mwagwaya Ndani, na Princess Fynick, waliokuja kwa mitoko ya kisasa. Kwa upande wa muziki, Reagan Dandy alikuwa miongoni mwa wanamuziki wachache kutoka Pwani waliobahatika kuhudhuria tukio hilo la hadhi ya kimataifa.
Jukwaa la Uchumi wa Ubunifu limeibuka kama jukwaa muhimu kwa kuvunja mipaka kati ya sanaa, biashara na teknolojia. Kupitia mikutano kama hii, wasanii, waunda maudhui na wadau wa sekta ya ubunifu wanapata nafasi ya kuunganishwa na fursa za kimataifa, kujifunza kuhusu ulinzi wa kazi zao, na kuelewa jinsi ya kujitegemea kiuchumi kupitia vipaji vyao. Kwa kizazi kinachotegemea mitandao na ubunifu kama njia ya kujieleza, majukwaa haya yanakuwa daraja kati ya ndoto na mafanikio halisi.
Kwa washiriki kutoka Pwani na sehemu nyingine za Kenya, kongamano hili halikuwa tu mahali pa kuonekana, bali pa kujifunza, kuunganishwa na kuchochewa kufikiria ubunifu kama ajira na biashara. Uwepo wa majina maarufu kama Ruby Kache, Bien, na waunda maudhui wengine wakubwa ulitoa motisha kwa vijana, huku ikithibitisha kuwa sanaa inaweza kuwa nguvu ya kiuchumi na chombo cha mabadiliko chanya katika jamii.