News
Kikao Cha Kujadili Jinsi ya Kusafisha Sumu ya Lead Eneo la Owino Uhuru Kimetibuka
Kikao cha kujadili jinsi kijiji cha Owino Uhuru katika eneo bunge la Jomvu kaunti ya Mombasa kitakavyosafishwa sumu ya Lead kimetibuka.
Hii ni baada ya wakaazi hao ambao ni waathiriwa wa sumu hiyo kutaka kikao hicho kilichojumuisha maafisa wa Mamlaka ya mazingira nchini NEMA na Wanaharakati wa kijamii kusitishwa.
Wakaazi hao wamelalaka kwamba kikao hicho kinatekelezwa kinyume cha sheria huku wakilalamikia kunyanyaswa na Mamlaka ya NEMA katika mchakato wa kupata fidia yao.
Wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika la Center for Justice, Governance and Environment Action Phyllis Omido wamesema tangu Mahakama iagize wakaazi hao walipwe fidia ya shilingi bilioni 2 hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha sheria katika Mamlaka ya NEMA Erastus Gitonga amesema zoezi la kusafisha mazingira ya Owino Uhuru litafanywa kwa hatua ikiwemo kufanya vipimo vya mchanga, maji na mimea katika eneo hilo ili kutathmini kiwango cha sumu.