Business
Wito kwa Wanawake Wafanyabiashara Jijini Mombasa Kuungana na Kukuza Masoko Yao
Wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogondogo katika jiji la Mombasa wametakiwa kuungana kupitia vikundi ili kuimarisha masoko ya bidhaa na huduma zao, si tu ndani ya nchi bali pia kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Collaboration of Women in Development (CWID), Bi. Betty Sharon, amesema kuwa licha ya juhudi kubwa zinazowekwa na wanawake katika sekta ya biashara ndogondogo, bado wanakumbwa na changamoto nyingi zinazokwamisha mafanikio yao.
Bi. Sharon amesisitiza haja ya kuwajengea uwezo wanawake hao kupitia mafunzo ya kibiashara na kuwawezesha kupata raslimali muhimu kama mitaji, teknolojia, na taarifa za masoko, ili kuongeza viwango vya uzalishaji na kuvuka mipaka ya soko la ndani.
Kwa upande wao, baadhi ya wanawake wafanyabiashara wakiongozwa na Bi. Beatrice Simiyu, wameitaka serikali pamoja na wahisani kuongeza juhudi katika kuwawezesha kwa kuwapatia ujuzi wa kibiashara na miundombinu bora ya kufanikisha biashara zao.