News

Rais Ruto amteua Amani Yuda Komora kuwa Mwenyekiti wa NPSC

Published

on

Rais William Ruto amemteua Amani Yuda Komora kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Huduma ya Polisi (NPSC) na Angeline Yiamiton Siparo kuwa mwanachama.

Uteuzi huo unafuatia mahojiano ya hivi majuzi yaliyofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kati ya Julai 1 na Julai 3 2025, baada ya kuorodhesha wagombea wanane wa uwenyekiti na 11 wa wajumbe.

Wawaniaji walitakiwa kuwasilisha kitambulisho halisi cha kitaifa, hati za masomo, na idhini halali kutoka kwa mashirika ya serikali.

Stakabadhi nyingine ilikuwa ni pamoja na nyaraka za mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA), tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC), fomu maalum kutoka kwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai (DCI), bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HELB) na ofisi yoyote iliyosajiliwa ya marejeleo ya mikopo.

Wale walio na shahadi ya digrii za mataifa ya kigeni walilazimika kuwasilisha barua za utambulisho kutoka kwa tume ya elimu ya vyuo vikuu.

Shughuli ya uteuzi ilianza mnamo mwezi Februari baada ya kujiondoa kwa tume ya awali, inayoongozwa na Eliud Kinuthia, ambaye muhula wake wa miaka sita ulimalizika mapema mwaka huu wa 2025.

Iwapo itaidhinishwa na Bunge, NPSC itajumuisha Komora kama Mwenyekiti na wanachama watano wakiwemo, Peris Muthoni Kimani, Edwin Cheluget, Benjamin Juma Imai, Collete Suda na Angeline Yiamiton Siparo

Komora ni naibu mwenyekiti wa zamani wa tume ya kutathmini mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa umma (SRC), na hapo awali alikuwa na majukumu ya juu ya rasilimali watu katika Mamlaka ya Bandari KPA na KRA.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version