National News
Wakaazi wa Jomvu Mombasa, Wanalalamikia Kucheleweshwa Kwa Fidia Yao
Wakaazi wa mtaa wa Owino Uhuru katika eneo bunge la Jomvu kaunti ya Mombasa, walioathirika na sumu ya madini ya kemikali ya Lead wanalalamikia kucheleweshwa kwa fidia yao.
Kulingana na wakaazi hao, mnamo Disemba 6 mwaka jana, Mahakama ya upeo nchini iliamua waathiriwa hao kufidiwa shilingi bilioni 2, lakini miezi 3 baadaye serikali haijaonyesha dalili yoyote ya waathiriwa hao kufidiwa.
“Zaidi ya watu 100 waliaga dunia kutokana na sumu ya madini hayo Lead na wengine wanaugua maradhi mbalimbali kama vile kuavya mimba, maradhi ya figo, ukosefu wa nguvu za kiume na maradhi mengine,” Wakaazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kimazingira la Center for Justice, Governance and Environmental Action Phyllis Omido, amesema huenda waathiriwa zaidi wakapoteza maisha iwapo hatua za dharua za matibabu hazitachukuliwa.
“Uwino Uhuru sai zaidi ya wananchi 100 walishaaga maisha na watoto, tumepoteza watoto zaidi ya 300 kwa vifo ambavyo viko vinahusiana na simu ya madini ya Lead na kwa hivyo wale ambao wamebaki wengi bado ni wagonjwa na wanahitaji matibabu na hizo fedha zitaenda kuwasaidia pakubwa,” Omido.
Itakumbwa kwamba tangu kesi hiyo ianze mwaka wa 2019 wakaazi hao bado hawajalipwa fidia yao licha ya Mahakama kuagiza familia hizo zilipwe fidia ya kima cha shilingi bilioni 1.3 na shilingi milioni 700 zaidi za kusafisha mazingira yao.