Business
Wadau wa utalii Watamu waunga mkono ada za maegesho mbugani
Wadau wa sekta ya Utalii eneo la Watamu kaunti ya Kilifi wameunga mkono pendekezo la shirika la huduma kwa wanyamapori nchini KWS la kutathmini upya ada za kuegesha magari mbugani.
Wadau hao walitoa shinikizo kuwa mabadiliko hayo yaainishwe na huduma zilizoboreshwa vile vile matokeo ya uhifadhi mbugani.
Wakizungumza wakati wa kikao cha kubadilishama maoni kuhusu suala hilo mjini Watamu, Patrick Changawa, mmoja wa wahudumu wa safari za kitalii, alisistiza kuhusu mchango muhimu unaotolewa na sekta ya utalii katika uchumi wa taifa.
Alipongeza KWS kwa kushirikisha wahusika wamaeneo hayo katika mchakato wa mashauriano.
“KWS imetuhamasisha kuhusu namna ada za uhifadhi zilizofanyiwa ukarabati zitakavyoanza kutekelezwa, mgao mkubwa wa fedha utatumika katika kuimarisha mbuga za baharini kupitia urejeshaji wa miamba ya matumbawe, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, na programu za kufikia jamii,” alisema Changawa.
Mkurugenzi msaidizi wa eneo la hifadhi ya pwani katika KWS Elema Hapicha alibainisha kuwa vikao sawa vya ushirikishwaji wa umma vinafanyika nchini kote ili kukusanya maoni kutoka kwa wadau.
“Wadau wa Watamu wametoa maoni muhimu kuhusu rasimu ya muundo wa ada ya uhifadhi,” Hapicha alisema.
Mapendekezo hayo yamejikita katika rasimu ya kanuni za uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori (Ada ya Ufikiaji na Uhifadhi) za 2025.
Taarifa ya Joseph Jira