News
Kaunti za Tanariver na Garissa zaathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi
Muungano wa mashirika ya kukabilina na athari za mabadiliko ya tabia nchi chini ya mpango wa WISER KENYA umetaja kaunti za Tanariver na Garissa kama zinazoathirika mara kwa mara na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkurugenzi wa mpango huo Phillip Omondi ambaye pia ni mwanasayasi wa masuala ya hali ya hewa, alidokeza kuwa kaunti hizo zimekuwa zikikumbwa na hali ya mafuriko na ukame kwa mda.
Akizungumza na Coco Fm, Omondi alisema kwa sasa wanaendelea na mikakati ya kuhamasisha jamii za sehemu hizo kuhusu namna ya kukabiliana na madhara hayo.
“Kaunti za Tanariver na Garissa ambako tunatekeleza mradi wa Wiser Kenya ni kaunti ambazo ziko katika hatari ya mafuriko na ukame, kwa hio serikali ya Uingereza imeunga mkono mpango huu kupitia FCDO ili tuweze kuutekeleza ili kusaidia jamii kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi yanayokumba kaunti hizo mbili
Mkurugenzi huyo alidokeza kuwa hatua hiyo inatokana na wito wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa António Guterres, wa kutaka ulimwengu kuhamasisha wananchi kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Alidokeza kuwa wanania ya kupeleka kampeni hiyo katika kaunti nyingine nchini katika siku zijazo.
Taarifa ya Joseph Jira