Business
KETRACO kuimarisha usalama wa chakula nchini
Shirika la usambazaji umeme nchini, KETRACO, limethibitisha dhamira yake ya kuimarisha usalama wa chakula, ukuaji wa kijani, na ushirikiano wa kieneo kupitia uekezaji mkubwa katika miundombinu ya umeme.
Katika maonesho ya Kimataifa ya kilimo ASK yanayoendelea kaunti ya Mombasa, KETRACO imeonyesha jinsi miundombinu yake ya umeme inavyowezesha kilimo cha kisasa na uzalishaji wa viwandani.
Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi mkuu, mhandisi Kipkemoi Kibias, KETRACO imekamilisha miradi 43 ya njia za kusafirisha umeme, huku mingine 29 ikitarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2028.
Kibias, alisema shirika hilo tayari limejenga zaidi ya kilomita elfu sita za njia za umeme wa msongo mkubwa, likiwa pia na vituo 46 vya kusambaza umeme na upanuzi wa mitambo 33.
Katika eneo la Pwani, Kibias alisema upanuzi wa mpango wa Green Energy Backbone umewezesha usambazaji wa kawi safi kwa asilimia 93, jambo lililopunguza utegemezi wa mafuta na kuchochea maendeleo ya biashara za kilimo, utalii na uchumi wa baharini.
Kibias alisema KETRACO inaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuunganisha Kenya na nchi jirani kupitia njia za kimataifa kama zile za Ethiopia, Tanzania na Uganda hatua zitakazowezesha biashara ya umeme Afrika Mashariki.
Taarifa ya Mwanahabari wetu