News
Wadau wa amani wabuni mbinu za kudhibiti utovu wa usalama
Wadau wa amani katika kaunti ya Kilifi wameishinikiza jamii kuzingatia amani na uwiano.
Wakiongozwa na Harold Mwatua ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya amani katika kaunti ya Kilifi, wadau hao walisisitiza haja ya uhusiano mwema baina ya maafisa wa usalama na jamii.
Mwatua alisema hali hiyo itasaidia sana katika kuimarisha usalama katika kaunti ya Kilifi kwa jumla.
“Nyinyi kama jamii mnawafahamu wale wote wanaotekeleza uhalifu, ushirikiano wenu na maafisa wa polisi utawezesha wahalifu kukamatwa na kushtakiwa” alisema Mwatua katika hafla ya kujenga uhusiano mwema baina ya maafisa wa usalama na raia kwenye uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi.
“Polisi ni binadamu kama wewe, ni mtu kama wewe, ni jirani na ndugu yako tuishi nao kwa amani na uwiano” aliongeza Mwatua.
Akiunga mkono kauli hiyo Mwenyekiti wa baraza la Wahubiri na Maimam ukanda wa Pwani CICC, Askofu Amos Lewa aliataka wakaazi kutojenga uadui na maafisa wa polisi iwapo wanapania kuona utovu wa usalama ukidhibitiwa.
Askofu Lewa pia aliwashinikiza wananchi kuzingatia amani hata katika kupigania haki huku akikashifu vikali maandamano ya vurugu na ghasia yaliyoshuhudiwa siku ya sabasaba jijini Nairobi.
Hafla hiyo iliwaleta pamoja maafisa wa usalama, maafisa tawala, mashirika ya kijamii na wananchi ili kutangaza Amani sawa na kujenga uhusiano mwema kati ya polisi na wananchi.
Taarifa ya Hamis Kombe