International News
Ghasia zatanda nchini Nepal licha ya marufuku ya kutotoka nje.
Marufuku ya kutotoka nje inaendelea kukiukwa nchini Nepal ambako ghasia za uharibifu wa mali na umwagikaji wa damu zinaendelea.
Serikali ya Waziri mkuu KP Sharma Oli, ilipinduliwa ndani ya masaa 48 baada ya kuzuka kwa maandamano hayo, ambapo waandamanaji waliokuwa na ghadhabu walivamia na kuteketeza makaazi ya Waziri mkuu Oli, pamoja na bunge la nchi hiyo.
Licha ya jeshi la nchi hiyo kutanganza hali ya tahadhari na marufuku ya kutotoka nje, Waandamanaji hao waliendelea kukiuka marufuku hiyo na kumiminika katika barabara za mji mkuu wa Kathmandu, huku wakiwashambulia maafisa wa usalama, lakini pia kulenga makaazi ya maafisa wakuu wa serikali, wakiwemo Wabunge na mawaziri huku wakiteketeza majumba na magari yao.
Kulingana na taarifa za maafisa wa usalama nchini humo, waandamanaji hao pia walivamia magereza na kuwaachilia huru jumla ya wafungwa elfu 13 katika kipindi cha wiki nzima ya maandamano.
Chanzo cha maandamano hayo yaliyoanzishwa na kizazi cha sasa cha Gen Z mapema wiki hii ni kukithiri kwa ufisadi serikalini mbali na sera duni zinazolenga kukandamiza vijana katika matumizi ya mitandao ya jamii.
Taarifa ya Eric Ponda