National News
Zoezi la Kuwapiga Msasa Makishna Wapya Kuanza Mwezi Machi
Jopo la uteuzi wa Makamishna wapya wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, limesema zoezi la kuwahoji na kuwapiga msasa wakenya waliotuma maombi ya kutafuta nafasi hizo litaanza rasmi mwezi Machi.
Mwenyekiti wa Jopo hilo Dkt Nelson Makanda amesema zoezi hilo litafanyika kwa wiki mbili kwani tayari mda wa kutuma maombi ya wale wanaotaka kujaza nafasi hizo ulikamilika Februari 15 mwaka huu na watu 1,848 wametuma maombi yao.
Dkt Makanda amewahakikishia wakenya kwamba zoezi hilo litakuwa huru na haki na litazingatia maadili, sheria na muongozo wa Katiba, huku akisema ni lazima wakenya wapate makamishna wa IEBC walio waadilifu na wachapa kazi.
Dkt Makanda amesisitiza kwamba taifa la Kenya linahitaji makamishna wa IEBC ambao wako tayari kufanikisha uchaguzi huru na haki, bila ya kushurutishwa na wanasiasa ama viongozi walio na ushawishi nchini.
Jopo hilo hata hivyo liko na mda wa hadi tarehe 25 mwezi Aprili mwaka huu, kukamilisha zoezi hilo na kuwasilisha majina ya makamishna wapya wa IEBC kwa rais William Ruto kabla ya kuwasilishwa bungeni ili kuidhinishwa rasmi.