News
ODM Na PAA, Wafanya mikutano tofauti kuhusu bunge la Kilifi
Mikutano miwili muhimu ya faragha imefanyika Jumatatu Juni 2 2025, kujadilia usimamizi wa vyama vya ODM na PAA ndani na nje ya Bunge la Kaunti ya Kilifi.
Taarifa za kuamika zasema, mikutano hiyo miwili ilikusudia kujadili matukio ya hivi majuzi katika Bunge la Kaunti ya Kilifi na usimamizi wake.
Mazungumzo ya Chama cha ODM yaliofanyika mjini Kilifi na kuhudhuriwa na viongozi wote waliochaguliwa, yalijikita katika tetesi za kumtimua Spika wa Bunge Teddy Mwambire, huku kukiwa na mpasuko baina ya wafuasi wa Spika Teddy Mwambire na kwa upande mwengine, wandani wa Gavana Gideon Mung’aro.
Tofauti kubwa za uongozi wa chama hicho cha ODM zilizuka tangu mchakato wa uchaguzi wa mashinani uliotibuka mwaka uliopita na uhasama huo sasa kuelekezwa ndani ya bunge la Kaunti kutaka kumuondoa Spika mamlakani kupitia kura ya kutokuwa na Imani naye ikidaiwa anahujumu serikali ya Gavana Mung’aro.
Pia mkutano huo ulijadili uwezo Mwakilishi Wadi wa Watamu Ibrahim Matumbo wa kuendelea kuwa kiongozi wa wengi Bungeni.
Kuna habari ambazo hazijathibitishwa kwamba huenda chama cha ODM kinataka kumuondoa Ibrahim Matumbo na wadhfa wake kuchukuliwa na Mwakilishi Wadi ya Ganda Oscar Wanje.
Kwa upande mwengine katika mkutano wa Chama cha PAA uliofanyika katika makao makuu ya chama eneo la Nyali kaunti ya Mombasa, yalijikita katika masuala ya usimamizi ndani ya bunge hilo na kumlenga zaidi kiongozi wa walio wachache katika bunge hilo la kaunti Tom Chengo.
Chengo ambaye pia ni Mwakilishi Wadi wa Tezo- kaunti ya Kilifi, anashtumiwa kwa kuhujumu upinzani ndani ya bunge hilo kutokana na usuhuba wake na Gavana Gideon Mung’aro.
Akizungumza na Cocofm kwa njia ya simu, Katibu mkuu wa Chama cha PAA, amnaye pia ni mbunge wa Ganze Kenneth Kazungu, alikiri kufanyika kwa mkutano huo, siku ya Jumatatu Juni 2, na kwamba mkutano huo ulikuwa kuweka sawa usimamizi na shughuli za chama ndani na nje ya bunge la kaunti.
Katika siku za hivi majuzi bunge hilo limeshuhudiwa mpasuko mkubwa wa kiutawala na kupelekea kutatizwa kwa vikao vya bunge vya kujadili masuala nyeti yanayogusia bejeti na usimamizi wa fedha na utekelezwaji wa miradi katika Wizara ya Afya.