News
Mbinu mpya ya kuwaua wakongwe Kilifi na Kwale yaibua hofu
Mashirika ya kutetea haki za binadamu eneo la pwani yameeleza wasi wasi wao kuhusu madai ya kuibuka kwa mbinu mpya ya mauaji ya wazee katika kaunti ya Kilifi na Kwale kutokana na mizozo ya umiliki wa ardhi.
Kwa mujibu wa afisa wa shirika la Haki Yetu John Obonyo, kwa sasa wahusika wanatumia mbinu ya kuteketeza moto nyumba za wazee sawa na kuwanyonga ili kuonekana wamejitoa uhai ili kupoteza ushahidi.
Obonyo hata hivyo alibaini kwamba watu hulipwa kati ya shilingi elfu tatu hadi shilingi elfu nne, ili kutekeleza mauaji hayo.
“Mauaji ya wazee yamezidi sana, yamezidi kwa misingi kwamba mbinu ambayo wazee wanapoteza uhai imebadilika, njia moja ni kuwa wanachomwa kwa nyumba kusudi wapoteze ushahidi, njia ya pili ni kuwa wananyongwa, na mtu ambaye amejinyonga nitofauti na yule ambaye amenyongwa, kwa hivyo ni njia tu yakupoteza ushahidi, lakini cha kusikitisha zaidi ni kuwa imekuwa na bei, sehemu za kilifi ukiwa na elfu 30 unatoa uhai”,alibaini Obonyo.
Hata hivyo Obonyo alipendekeza wazazi kuandika wosia kwa familia zao wakati wa uhai wao ili kuepuka mizozo kama hiyo kushuhudiwa.
Kaunti za Kilifi na Kwale zimekuwa zikiongoza kwa visa hivyo ambapo wakongwe wamekuwa wakiuawa kwa tuhuma za ushirikina, japo ilibainika kuwa mauaji hayo yanachangiwa na wanafamilia kutaka kurithi mali.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.