Rais William Ruto amewateua watu 15 kuwa Majaji wa Mahakama ya rufaa baada ya kuhojiwa na kupigwa msasa na Makamishna wa Tume ya huduma ya Mahakama nchini JSC.
Watu hao wanajumuisha, Jaji wa Mahakama kuu Enock Chacha Mwita, Wakili Katwa Kigen, Johnson Okoth Okello, Lilian Paul, Munyao Sila, Byram Ongaya, Brown Murungi Kairaria, na Stephen Andersen Radido Okiyo.
Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Mamlaka ya IPOA Ahmed Issack Hassan, Hedwig Imbosa Ong’udi, Mathews Nduma Nderi, Linnet Mumo Ndolo, Lucy Mwihaki Ngujuna, Samson Odhiambo Okongo na Rachel Chepkoech Ngetich.
Katika chapisho la gazeti rasmi la serikali, Rais Ruto kwa kuzingatia kipengele cha Katiba ya 166 ibara ya kwanza (b) kinachompa mamlaka ya kuwateua majaji, Kiongozi wa nchi ametumia kipengele hicho na kutekeleza jukumu lake la kuwateua majaji hao 15.
Hata hivyo baada ya kuapishwa, watahitajika kuanza majukumu yao Mahakamani, wakilenga kuziba pengo la uchache wa Majaji kwenye idara ya Mahakama nchini.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi.
