Viongozi wa kidini katika eneo bunge la Kinango wamejitokeza na kuishinkiza serikali ya kaunti ya Kwale kuweka mikakati bora ya kukabiliana na kiangazi kikali katika eneo hilo.
Viongozi hao wakiongozwa na Katibu wa Maimam kaunti ya Kwale Faraj Abubakar Omar walisema badala ya kusubiri misaada ya dharura kutoka kwa wahisani mbalimbali itakuwa bora zaidi iwapo serikali ya kaunti hiyo itawekeza katika miradi ya kuhifadhi maji.
Omar alisema licha ya eneo hilo kuwa na vyanzo vya maji viongozi wa kiserikali wamekosa mifumo bora ya kuhifadhi maji, akisisitiza haja ya kukamilishwa kwa ujenzi wa mabwawa ili kuwasaidia wakaazi kufanikisha Kilimo nyunyizi.
Aidha alisema iwapo viongozi watawekeza zaidi katika ujenzi wa mabwawa basi eneo hilo litakuwa na uzalishaji wa chakula cha kutosha na kukabiliana na changamoto za uhaba wa chakula na ukame.
“Eneo ambalo ni kame huwa ni kame watu mpaka wafahamu hapo na badala yake kuwe na kilimo mbadala kwa hivyo ni ombi haya mabwawa ambayo yameanza yafanyiwe haraka iwezekanavyo yakamilike ili wananchi wa maeneo kama hayo badala ya kulia kila siku na njaa tuweze kulima na kuzalisha chakula”, alisema Omar.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
