Ogamba awaonya walimu wakuu dhidi ya kuwarudisha wanafunzi nyumbani

Ogamba awaonya walimu wakuu dhidi ya kuwarudisha wanafunzi nyumbani

Waziri wa Elimu nchini Julius Migos Ogamba amewaonya Walimu wakuu dhidi ya kuwarudisha nyumbani wanafunzi ambao hawana karo ama sare za shule, akisema watakaopatikana watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufutwa kazi.

Waziri Ogamba alisema sera ya serikali ya asilimia 100 ya wanafunzi kujiunga na shule inaendelezwa, akidoeza kwamba kufikia sasa ni asilimia 8 pekee ya wanafunzi ambao bado hawajajiunga na shule za Sekondari ya juu nchini.

Akizungumza na wadau wa sekta ya elimu jijini Nairobi, Ogamba aliwataka Walimu wakuu wa shule za Sekondari ya juu kuhakikisha wanatumia raslimali walizonazo shuleni ili kuhakikisha hakuna Mwanafunzi anakosa kujiunga na gredi ya 10.

“Tunashirikiana na waajiri wa walimu TSC, na Mwalimu wakuu watakaowarudisha wanafunzi wa gredi ya 10 nyumbani eti hawana karo ama sare za shule tutawachukulia hatua kwa sababu haina haja ya kurudisha wanafunzi wawili ama watatu kwa kukosa sare za shule, hiyo haitakubalika”,alisema Waziri

Wakati huo huo alidokeza kwamba tayari serikali imesambaza asilimia 50 ya fedha za kusimamia shughuli za masomo ya kalenda ya mwaka 2026, ili kuhakikisha shule hazikumbwi na changamoto.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi