Maafisa wa Kliniki watia saini mkataba wa kurejea kazini

Maafisa wa Kliniki watia saini mkataba wa kurejea kazini

Baraza la magavana, bodi ya huduma za umma kaunti ya Mombasa pamoja na Muungano wa maafisa wa Kliniki nchini (KUCO), wametia saini mkataba wa makubaliano ya kurejea kazini. 

Mweyekiti wa kamati ya ukusanyaji wa rasilimali na ushirikiano katika baraza la magavana ambaye pia ni Gavana wa Nandi Stephen Sang, Mwenyekiti wa Bodi ya huduma za umma kaunti ya Mombasa Farida Abdallah, pamoja na viongozi wa Muungano wa maafisa wa Kliniki wameshuhudia kutiwa saini kwa mkataba huo.

Makubaliano hayo yamehitimisha rasmi mgomo wa kitaifa wa siku 36 wa maafisa wa kliniki, uliyokuwa umesitisha shughuli za utoaji wa huduma za afya katika vituo vya afya vya umma kote nchini.

Mchakato wa mashauriano, uliotegemea mazungumzo na ujenzi wa maridhiano, ulihitimishwa kwa ahadi ya Serikali za kaunti kutekeleza kikamilifu maazimio yaliyokubaliwa, ikiwemo kutiwa saini kwa mkataba wa makubaliano wa malipo nchini CBA, unaotarajiwa kufanyika Februari tarehe 2 mwaka huu.

Mpangilio wa kurejea kazini unafungua njia ya kurejelewa kwa huduma muhimu za afya na unaimarisha dhamira ya uongozi wa kaunti katika kuimarisha mifumo ya afya ya umma.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi