Polisi waimarisha doria eneo la Hulugho kufuatia shambulizi la kigaidi

Polisi waimarisha doria eneo la Hulugho kufuatia shambulizi la kigaidi

Idara ya usalama nchini imesema imeimarisha doria na operesheni za kiusalama zinaendelea katika kaunti ya Garissa kufuatia shambulio la kigaidi lilitekelezwa katika eneo la Hulugho na kusababisha vifo vya watu wawili.

Idara hiyo ilisema inaendelea kuwasaka waliohusika na mauaji hao, ikisema eneo hilo sasa limedhibitiwa na operesheni za kiusalama zinaendelea kwani maafisa wa usalama wametuma eneo hilo.

Idara hiyo kupitia Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja iliwahakikishia wakaazi wa kaunti hiyo ya Garissa usalama wa hali ya juu na kuwahimiza kudumisha utulivu na kuwa macho.

Hata hivyo baadhi ya walimu wanaohudumu katika shule za kaunti hiyo ikiwemo shule ya msingi ya Hulugho, wameitaka serikali kupitia Tume ya kuajiri walimu nchini TSC kuwapa uhamisho wa haraka ili kuokoa maisha yao.

“Chifu wa eneo hilo na Mwalimu wenzetu walitolewa ndani ya nyumba na kupigwa risasi hadi kuuwawa, na sisi tunaiambia Tume ya TSC itupatie uhamisho, sisi hata hatujui tulale wapi, tuko na wasiwasi kuhusu usalama wake, tunaomba tafadhali serikali tusaidieni jamani”, alisema Mwalimu

Chifu wa eneo hilo, Abdifatah Gani, pamoja na Mwalimu wa Shule ya msingi ya Hulugho, Stephen Musili, ni kati ya waliouawa katika shambulio hilo la usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu Januari 26, 2026.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi