Murkomen, aagiza uchunguzi kufanywa kuhusu kuvamiwa kwa Gachagua Kanisani

Murkomen, aagiza uchunguzi kufanywa kuhusu kuvamiwa kwa Gachagua Kanisani

Waziri wa Usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amelaani vikali tukio la kuvurugwa kwa ibada ya Jumapili katika Kanisa la ACK, Witima eneo la Othaya, kaunti ya Nyeri, ambayo Kinara wa Chama cha DCP Rigathi Gachagua alikuwa amehudhuria.

Ibada hiyo ilivurugika baada ya watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi waliokuwa wamevaa kiraia kurusha vitoa machozi na kufyatua risasi.

Murkomen alisema kuvunjwa kwa utulivu wa waumini Kanisani ni kinyume cha maadili ya kidemokrasia, akibainisha kwamba tukio hilo ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya uhuru na demokrasia.

Waziri Murkomen alisema tayari amefanya mazungumzo na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja, ili kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanywa mara moja na waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huo huo aliwataka wakaazi wa kaunti ya Nyeri kudumisha utulivu, akisema vikosi vya usalama vinaendelea kushughulikia suala hilo.

Hata hivyo Kinara wa DCP Rigathi Gachagua alimshtumu Rais Ruto, akisema kwamba ana njama ya kumuangamizi kutokana na misururu ya mashambulizi dhidi yake ambayo yamekuwa yakitekelezwa na maafisa wa polisi wasiovaa sare za kazi.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi