Waziri wa Fedha nchini John Mbadi amesema serikali inalenga kuwaondolea ushuru wa PAYE wakenya wanaopata mshahara wa chini ya shilingi elfu 30 kwa mwezi huku wale wanaopata mshahara wa shilingi elfu 30 hadi laki tano wakitozwa ushuru wa asilimia 25.
Waziri Mbadi alisema hatua hiyo inalenga zaidi ya wakenya milioni 1.5 na hivi karibuni atawasilisha mswada bungeni ili pendekezo hilo liangaziwe na sheria ya ushuru ifanyiwe marekebisho kabla ya kupitishwa kwa mswada wa fedha wa mwaka wa 2026.
Waziri Mbali aliyasema hayo wakati wa kikao cha kukusanya maoni ya umma katika kaunti ya Meru ambapo alikuwa amefanya kikao cha mazungumzo na Rais William Ruto na kuafikiana kuhusu pendekezo hilo.
Waziri huyo wa fedha nchini aliongeza kwamba mswada huo pia utajumuisha pendekezo la kupunguza ushuru wa PAYE kwa asilimia 5 kwa wakenya wanaopokea mshahara wa kati ya shilingi elfu 32,050 kwa mwezi hadi shilingi laki tano, akisema punguzo hilo la asilimia 5 litasaidia wakenya kumudu gharama ya maisha.
“Tumekubaliana na Rais kwamba wananchi wenye kipato cha chini wanapaswa kupata nafuu kwenye mishahra yao kwani idadi kubwa ya wananchi wanapitia hali ngumu ya maisha na hatua hii itasaidia wakenya wengi kuwa na pesa mfukoni. Sidhani kama kuna mbunge yeyote atapinga pendekezo hilo”, alisema Mbadi.
Waziri huyo wa fedha alishikilia kwamba hatua hiyo inalenga kupunguza mzingo wa ushuru kwa wakenya wa kipato cha chini na cha kati na kuwasaidia kujikimu katika kipindi hiki cha gharama ya juu ya maisha.
Kwa sasa kikomo cha ushuru wa PAYE kinaathiri wakenya wengi wenye kupokea mshahara wa kuanzia shilingi elfu 24, akisema wataalamu wamebaini kwamba kupunguzwa kwa ushuru kutachangia matumizi ya nyumbani kuwa ya usawa na kusaidia kuimarisha uchumi unaokabiliwa na mahitaji duni.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
