Polisi waanzisha uchunguzi dhidi ya mafunzo potovu Chamari

Polisi waanzisha uchunguzi dhidi ya mafunzo potovu Chamari

Idara ya usalama katika eneo la Magarini kaunti ya Kilifi imeanzisha uchunguzi kuhusu baadhi ya nyumba za ibada zinazohushwa na mafunzo ya Imani potovu katika eneo la Chamari eneo la Magarini.

Naibu Kamishna wa eneo hilo Michael Ololtuaa alisema baadhi ya wachungaji wamekuwa wakiwashurutisha waumini wapande juu ya miti iliyoko katika mazingira ya makanisa wakiamini kwamba matatizo yao yataisha.

Ololtuaa alisema serikali haitakubali mafunzo kama hayo kuendelea kushuhudiwa makanisani, akisema makanisa yatakayopatikana yakiendelea mafunzo hayo yafungwa na wachungaji kupokonywa vibali.

“Mambo ya kupanda juu ya miti na kuanza kutabiri mambo ya kupotosha watu kiimani kama serikali hatutakubaliana na suala hilo na kutafunga hayo makanisa na kuwachukulia hatua wachungaji wanaohusika na mafunzo potovu”, alisema Ololtuaa.

Kwa upande wake Kiongozi wa wachungaji katika eneo la Adu Johnson Kaingu amesema wachungaji katika eneo hilo wameanza kupokea mafunzo bora ya kidini ili kudhibiti mafunzo potovu kwenye nyumba za ibada.

“Tumeanzisha mafunzo kwa wachunguji wa maeneo haya na tutahakikisha mafundisho hayo yanaendelea ili kuzuia waumini kupotoshwa na imani potovu”, alisema Kaingu.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi