News
Kongamano la mabadiliko ya hali ya anga lafanyika Mombasa
Mratibu wa Kongamano la kimataifa linaloangazia masuala ya mabadiliko ya hali ya anga, INTER- GOVERNMEMTAL PANEL ON CLIMATE CHANGE, Patricia Nying’uro amesema jamii inasalia kuwa kiungo muhimu katika harakati za kuangazia mfumo wa mabadiliko ya hali ya hewa.
Kufuatia hilo, Nying’uro alitoa wito kwa wadau wa mazingira kuwekeza zaidi na kuhakikisha kila mmoja anashiriki ipasavyo katika kudhibiti mabadiliko hayo.
Nying’uro alisema Kongamano ambalo linaendelea katika kaunti ya Mombasa, linaangazia masuala ya mabadiliko ya hali ya anga na limewekeza kutambuliwa na jamii katika mikakati hiyo.
Akizungumza katika eneo la Shanzu wakati wa majadiliano hayo, Nying’uro alisema jumla ya mataifa 56 kati ya mataifa 195 yanayoshiriki kwenye mchakato wa kuweka mipango, sera na mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa yanakongamana eneo la Shanzu ili kuanisha ripoti ambayo itatoa muongozo rasmi wa kuangazia makali ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Wakati huohuo, Nying’uro alisema pia kongamano hilo la kimataifa lina umuhimu mkubwa kwa taifa hili kwani Kenya itahusishwa moja kwa moja katika kupangilia sera za kimataifa za kudhibiti athari ya mabadiliko ya hali ya anga.
Taarifa ya Janet Shume