News
Miili iliyosalia Shakahola kuzikwa na Serikali
Huenda serikali ikalazimika kuizika miili ya watu waliofariki dunia eneo la Shakahola, Magarini kaunti ya Kilifi baada ya zoezi la kuitambua miili hiyo kusitishwa.
Waziri wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen alisema kuwa miili hiyo itazikwa katika sehemu moja na kisha sehemu hiyo kutengwa kama hifadhi ya kumbukumbu kwa waathiriwa.
Murkomen alisema kuwa zoezi hilo limekwama kutokana na familia nyingi kutojitokeza kuitambua miili hiyo akisema kuwa huenda ikawa miili mingi iliyopo kwa sasa sio ya watu waliokuwa wakaazi na wenyeji wa Kilifi.
“Hii miili sio ya Kilifi kaunti pekee bali Kenya nzima, Baringo, Vihiga, Siaya, Kisumu, maeneo hayo yote na sasa jamaa za watu hao hawajui kama watu waliopotea ni kweli walienda Shakahola na wakakufia huko, ndio maana hawajitokezi ili kufanyia sampuli za vinasaba”, alisema Murkomen
Kufuatia hilo Murkomen alihoji kuwa huenda serikali ikatumia njia mbadala kukamilisha zoezi hilo
Taarifa ya Hamis Kombe