News
IEBC yasistiza usalama kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, Erastus Ethekon, amesisitiza umuhimu wa usalama katika maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.
Akizungumza kwenye mkutano wa ushirikiano na vitengo vya usalama kutoka kaunti za Mombasa, Kwale na Kilifi, Ethekon alisema tume ya IEBC imeendelea kushirikiana kwa karibu na vitengo hivyo tangu mwaka 2013, kuhakikisha chaguzi zinakuwa za amani, haki na uwazi.
Hata hivyo Ethekon alikiri kuwepo kwa changamoto kama vile uhaba wa fedha, vitisho vipya vya kiusalama, ukiukaji wa haki za binadamu, pamoja na ghasia za kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana wakati wa chaguzi.
Mwenyekiti huyo vile vile alisema usalama wa uchaguzi si wa siku ya kupiga kura pekee, bali ni mchakato unaopaswa kuzingatiwa kuanzia usajili wa wapiga kura hadi kutangazwa kwa matokeo.
Kwa upande wake, kamishna wa IEBC Anne Nderitu alisema tume ya IEBC imeweka mikakati kuhakikisha chaguzi ndogo zipatazo 24, zinafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria.
Taarifa ya Mwanahabari wetu