Sports

Sinner na Alcaraz Wakutana Tena Fainali ya US Open Baada ya Muitaliano Kufuzu Fainali ya Tano Mfululizo ya Grand Slam

Published

on

Bingwa taji la US Open mchezo wa tenisi Jannik Sinner anatarajia mechi ya kipekee na “maalum” atakapokutana na mchezaji wa pili duniani Carlos Alcaraz raia wa Uhispania kwenye fainali ya wanaume ya US Open baada ya Muitaliano huyo kufuzu kwa fainali yake ya tano mfululizo ya Grand Slam siku ya Ijumaa.

Sinner alimshinda Felix Auger-Aliassime kwa seti 6-1, 3-6, 6-3, 6-4 na sasa analenga taji lake la tano la Grand Slam baada ya kujiunga na Rod Laver, Roger Federer na Novak Djokovic kama wanaume pekee kufika fainali zote nne za Grand Slam katika msimu mmoja.

“Nadhani kufika fainali tano mfululizo za Grand Slam ni jambo kubwa. Uthabiti na kujiweka katika hatua za mwisho za mashindano makubwa tuliyonayo, ni kitu cha kushangaza,” alisema Sinner.

Nafasi yake ya kwanza duniani itakuwa hatarini Jumapili wakati atakapokutana na Alcaraz kwa mara ya tatu mfululizo katika fainali ya Grand Slam.

Sinner mwenye umri wa miaka 24 alitwaa mataji ya Australian Open na Wimbledon msimu huu lakini alifungwa na Alcaraz mwenye miaka 22 katika pambano kali la seti tano kwenye French Open.

“Uwanjani tunapenda kukutana, unajua, kwa sababu kutokana na nafasi zetu kwenye viwango, inamaanisha tunafanya vizuri kwenye mashindano,” alisema Sinner.

Watakutana tena US Open kwa mara ya pili. Mchuano wao wa kwanza ulikuwa robo-fainali ya 2022, pambano kubwa lililounda ushindani wao.

“Jumapili ni siku maalum sana na fainali ya kushangaza tena,” alisema Sinner. “Ninahisi ushindani wetu ulianza hapa kwa kucheza mechi ya ajabu. Sasa sisi ni wachezaji tofauti, wenye kujiamini zaidi pia.”

Miaka mitatu iliyopita, Alcaraz ndiye aliyeshinda baada ya pambano lililodumu saa 5 na dakika 15 na kumalizika kabla ya saa 9 alfajiri huko New York, na Mspaniola huyo akaenda kunyanyua taji lake la kwanza la Grand Slam kwenye mashindano hayo.

Sinner analenga kumshinda Alcaraz Jumapili kwa kutwaa taji lake la tano la Grand Slam. Mafanikio hayo yamejengwa zaidi kwenye ushindi wa mechi 27 mfululizo za Grand Slam kwenye uwanja wa hard court.

Analenga kuwa mwanaume wa kwanza kutetea taji la US Open tangu Federer alipochukua la mwisho kati ya mataji yake matano mfululizo mwaka 2008.

Mkanada Auger-Aliassime alikuwa akijaribu kufuzu kwa fainali yake ya kwanza ya Grand Slam baada ya kufika nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu safari yake hadi hatua hiyo hiyo kwenye US Open mwaka 2021.

“Sina majuto. Nilicheza kwa njia yangu. Nilicheza mchezo wangu. Unajua, kwa namna fulani unaishi na kufa na maamuzi yako,” alisema Auger-Aliassime.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version