Uncategorized
Kaunti ya Mombasa Yatakiwa Kuchukua Hatua za Dharura Kusafisha Soko la Marikiti
MOMBASA – Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuondoa taka zilizorundikana katika soko la Marikiti, hatua inayolenga kupunguza hatari ya kiafya na uvundo unaosababishwa na uchafu huo, hasa katika msimu huu wa mvua.
Akizungumza na wanahabari, Mwenyekiti wa soko hilo, Muhammad Ali, amesema kuwa hali ya uchafu sokoni hapo imefikia kiwango cha kutisha, huku baadhi ya wanunuzi wakikwepa kufika sokoni humo kutokana na harufu kali na mazingira yasiyovutia.
“Tumejaribu kuwasiliana na serikali ya kaunti mara kadhaa kuhusu suala hili, lakini hadi sasa hatujapata suluhisho la kudumu. Taka zimejaa kila kona ya soko, na hali hii si tu inatishia afya ya wananchi, bali pia inasababisha hasara kwa wafanyabiashara,” alisema Ali.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mvutano kati ya serikali ya kaunti na baadhi ya wafanyabiashara kuhusu ni nani anapaswa kukusanya taka umekuwa kizingiti kikuu katika kutatua changamoto hiyo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni jukumu la moja kwa moja la serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa huduma za ukusanyaji taka zinatolewa kwa wakati katika masoko yote ya umma.
“Hili si suala la kubebana lawama. Serikali ya kaunti ina wajibu wa kuhakikisha mazingira safi na salama kwa wafanyabiashara na wateja,” aliongeza.
Wafanyabiashara sokoni Marikiti wanasema hali hiyo imeathiri sana mapato yao, huku wakiitaka kaunti kuingilia kati na kurejesha heshima ya soko hilo linalohudumia maelfu ya wakazi wa Mombasa kila siku.