News
Karua na Mutunga, waishtaki Tanzania
Aliyekuwa Jaji mkuu nchini Willy Mutunga pamoja na Kinara wa chama cha People’s Liberation Party Martha Karua wameishtaki serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).
Mutunga na Karua pamoja na Wanaharakati wengine wanane wa haki za binadamu akiwemo Hussein Khalid, Gloria Kimani, Lyn Nguji, Hanifa Adan, Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire walishtumu serikali hiyo kwa kuwazuia kuingia nchini humo.
Wanane hao walidai kwamba haki zao zilikiukwa kwa kuondolewa kwa nguvu nchini humo huku wakidai kwamba serikali ya Tanzania ilikiuka mikataba ya Kikanda.

Jumba la Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo na Mahakama ya EACJ
Wanane hao sasa wanaitaka Mahakama hiyo kuishurutisha serikali ya Tanzania kuondoa alama zozote hasi za uhamiaji kwenye Pasipoti zao za usafiri na kuwalipa fidia maalum kwa gharama walizopata wakitafuta ushauri wa kisaikolojia kutokana na msongo wa mawazo na kihisia.
Haya yanajiri wiki chache baada ya Willy Mutunga, Martha karua na Wanaharakati wanane wa kutetea haki za kibinadamu kutoka nchini Kenya na Uganda kutimuliwa nchini humo baada ya kuzuiliwa.
Wakenya hao walikuwa wamezuru nchini kusikiliza na kumuakilisha Kiongozi wa chama cha upinzani nchini humo Tundu Lissu katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Lissu ambaye anakabilia na kesi ya uhaini pamoja na tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo yupo rumande akisubiri kesi yake kutajwa tena tarehe 16 mwezi Juni 2025.
Taarifa ya Elizabeth Mwende