News
Chibule, apendekeza adhabu kali kwa wanaoendeleza dhulma za kijinsia
Naibu gavana kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule, amependekeza adhabu kali kwa watu wanaotekeleza visa vya dhulma za kijinsia katika jamii.
Chibule alisema visa vya dhulma za kijinsi dhidi ya watoto vimekithiri katika jamii hasa kaunti ya Kilifi, akiahidi ushirikiano wa hali ya juu na wadau mbalimbali ili kukomesha visa hivyo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya hamasa kuhusu dhulma za kijinsia katika uwanja wa Bofa Youth mjini Kilifi, Chibule alisema ili kufanikisha ndoto ya mtoto wa kike ni lazima haki zao za kimsingi zilindwe.
“Kwa ambao wanadhulumu mtoto wa kike na kiume, kwa wale ambao wanaingia misuli kwa misuli wanafaa kuwekwa gerezani kabisa”, alisema Chibule.
Wanaharakati wa kijamii wapinga unyanyasaji wa kijinsi, Kilifi
Kwa upande wake Mwakilishi wa kike kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu aliyeandaa hafla hiyo kupitia hazina ya kitaifa ya NGAAF na kutoa hundi ya kima cha shilingi milioni 1.6 kwa makundi 14, alisisitiza hamasa zaidi kwa jamii kuhusu jinsi ya kukomesha visa hivyo.
“Ni jukumu letu la kuwaeleza hawa watu watambua jinsi ya kuripoti hizi kesi, yani kwa mfano umedhulumiwa ni wapi pa kuanzia na hatua hii itakomesha hizi visa”, alisema Mbeyu.
Naye Mzee wa mataa wa Kiwandani mjini Kilifi Elina Nyevu alisema visa vya dhulma za kimapenzi vimekithiri mno katika mtaa huo, akipendekeza hamasa zaidi kwa jamii.
“Hapa kwetu Kiwandani visa vya dhulma za kijinsia ni vingi sana, kuna ulevi na ukosefu wa ajira ambao umechangia utumiaji wa Mihadarati na unyanyasaji wa watoto wadogo kimapenzi, alisema Elina.
Hata hivyo katika halfa hiyo baadhi ya watoto waliopitia madhila hayo hasa ubakaji wameelezea masaibu waliopitia japo haki yao kupitia idara ya usalama walikosa kufaulu.
Taarifa ya Lolani Kalu.