News
Shehena ya Chanjo za Polio na BCG zawasili nchini.
Shehena ya dozi milioni 3.2 za chanjo ya ugonjwa wa polio na dozi milioni 3 za chanjo ya BCG inayotumiwa kuzuia ugonjwa wa kifua kikuu zimewasili nchini.
Kuwasili kwa chanjo hizo kumewapunguzia mahangaiko na wasiwasi wazazi ambao wamekuwa wakisubiri chanjo hizo kwa zaidi ya miezi 3.
Kwa sasa wizara ya afya nchini inazindua kampeni ya kitaifa ya kuhakikisha watoto wote waliokosa chanjo hizo wanazipokea.
Waziri wa afya Aden Duale amesema kampeni hiyo inatarajiwa kuanza mnamo juni tarehe 15 mwaka huu kote nchini.
Ili kusaidia maelfu walioathirika, wahudumu wa afya ya jamii watasaidia kuwatambua na kuwaelekeza akinamama kwenye kliniki zilizoko karibu.
Kulingana na mkurugenzi wa afya nchini daktari Patrick Amoth, takriban watoto elfu 80 hawakupata chanjo kufuatia uhaba ulioshuhudiwa.
Kaunti kumi na mbili hazikuwa na chanjo hizo muhimu huku maeneo ya mipakani na khambi za wakimbizi yakiathirika zaidi.
Taarifa ya Joseph Jira