News
Hofu ya kupoteza ajira kwa wafanyakazi wa KEMRI.
Kaimu Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa matibabu nchini, KEMRI, Prof. Elijah Songok amesema huenda maelfu ya wananchi wanaofanya kazi kwenye taasisi hiyo kote nchini wakakosa ajira.
Hii ni kufuatia ukosefu wa ufadhili kutoka kwa mashirika ya kimataifa ikiwemo lile shirika la misaada la Marekani la USAID.
Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi baada ya kufanya kikao cha faragha na kamishna mkuu wa Uingereza ,Prof. Songok alisema hali hiyo pia huenda ikaathiri pakubwa utoaji wa huduma za matibabu.
Prof. Songok alidokeza kuwa serikali ya Uingereza imeahidi kuimarisha ufadhili wake baada ya kuongeza kandarasi ya miaka 7 zaidi na taasisi ya KEMRI, huku akisisitiza haja ya ufadhili kuongezwa.
Wakati huo huo Prof. Songok pamoja na mwenyekiti wa bodi ya usimamizi wa KEMRI, Dkt. Abdillahi Ali walihoji kwamba kupitia idara husika, KEMRI itaruhusiwa kuuza bidhaa kama vile dawa zinazobuniwa baada ya kufanyiwa utafiti ili kuwezesha taasisi hiyo kujisimamia yenyewe pasi na kutegemea misaada.
Taarifa ya Hamisi Kombe