News
IPOA: Watu 20 walifariki katika vituo vya polisi mwaka huu
Mamlaka ya kuchunguza utendakazi wa maafisa wa polisi nchini IPOA, imetoa tahadhari kwa taifa kutokana na ongezeko la vifo vya wakenya vinavyotokea katika vituo vya maafisa wa Polisi nchini.
Katika ripoti iliyotolewa na IPOA, takriban watu 20 wamefariki wakiwa chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi katika kipindi cha miezi minne pekee iliyopita.
Mwenyekiti wa IPOA Issack Hassan, amesema Mamlaka ya IPOA haijawakamata washukiwa wa visa hivyo kutokana na mamlaka hiyo kutokuwa na uwezo, akisema washukiwa wote wanaohusishwa na kesi hizo wanachukuliwa kama wahalifu.
“Tumenakili visa visivyopungua 20 katika kipindi cha miezi minne pekee kwamba watu hawa walipoteza maisha yao ndani ya seli zetu na kunaendelea na uchunguzi, kesi hizo zitafikishwa kwa Ofisi ya ODDP na wahusika watafunguliwa mashtaka”, alisema Hassan.
Hassan amesema kufikia sasa maafisa wa polisi 17 wamehojiwa kuhusiana na matukio hayo ikiwemo wale waliomkamata Albert Ojwang pamoja na mashahidi 6, akisema haki kwa familia za wale waliopoteza wapendwa wao itapatikana.
Mwenyekiti huyo wa IPOA, ameyasema hayo alipofika mbele ya kamati ya bunge la kitaifa kuhusu usalama, akisema Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Eliud Lagat pia atafika mbele ya Mamlaka ya IPOA kuandikisha taarifa kuhusu kifo cha Ojwang.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi