International News
Iran Yafanya Mashambulizi Qatar
Katika juhudi za kulipiza Mashambulio ya jeshi la Marekani dhidi ya vituo vya Nyuklia, Iran siku ya Jumatatu Juni 23, imevurumisha makombora na kushambulia kambi ya jeshi la Marekani ilioko Qatar, Milki za Kiarabu.
Mashambulio hayo ya hivi punde katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati, yanazidisha wasiwasi katika eneo hilo la Ghuba.
Muda mfupi baada ya shambulio hilo, Bahrain na pia Qatar ambazo ni makao ya kambi ya kikosi cha 5th Fleet cha Jeshi la Marekani, zilisitisha mara moja safari zote za ndege katika anga zao.
Makombora hayo ya Iran yalilenga kambi ya kijeshi ya Al Udeid nchini Qatar ingawa jeshi la Marekani liliweza kuyategua makombora hayo kabla ya kusababisha maafa makubwa.
Hakuna habari zozote za majeruhi zilizotolewa kufikia sasa.
Shirika la Habari la AP liliripoti kwamba, Iran imetoa taarifa kudai kwamba makombora yaliyovurumishwa yanauzani sawa na yale yaliyotumiwa na Jeshi la Marekani kuharibu vituo vyake vya Nyuklia huko Fordow.
Hata hiyo Iran ilisema kwamba ililenga kambi hiyo la Al Ufeid ambayo iko mbali kidogo na makaazi ya watu.
Aidha makombora hayo pia yalilenga kambi ya makaazi ya jeshi la Marekani la Ain Al-Assad iliyoko eneo la magharibi mwa Iraq.
Kiongozi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alionya kwamba, Mashambulio hayo ya Marekani yatakuwa na athari kubwa za kiusalama sio tu kwa Marekani bali pia eneo la Mashariki ya Kati.
Isreal pia ilizidisha Mashambulio yake dhidi ya Iran kulenga gereza ambalo yaaminika limekuwa likitumiwa kuwafungia wanaharakati wa kisiasa nchini humo.