Rais wa Malawi Chakwera akubali kushindwa katika uchaguzi

Rais wa Malawi Chakwera akubali kushindwa katika uchaguzi

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amekubali kushindwa katika uchaguzi wa wiki jana, akisema katika hotuba yake kwa taifa kwamba ni wazi mpinzani wake Peter Mutharika alikuwa na “uongozi usioweza kushindwa”.

Mchungaji huyo wa zamani alichukua mamlaka katika uchaguzi wa 2020 alipomshinda rais wa wakati huo Mutharika, ambaye ni mtaalamu wa sheria za kikatiba kutoka chama cha Democratic Progressive Party.

“Dakika chache zilizopita, nilimpigia simu profesa Mutharika kumtakia heri,” Chakwera alisema saa chache kabla ya halmashauri ya kusimamia uchaguzi kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Septemba 16, 2025.

Kabla ya tangazo hilo, “ilikuwa wazi kwamba mpinzani wangu Peter Mutharika ana uongozi usioweza kushindwa juu yangu,” alisema Chakwera, mwenye umri wa miaka 70, kutoka Chama cha Malawi Congress (MCP).

Hali mbaya ya uchumi ilitawala uchaguzi katika nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika, huku wakosoaji wakimshutumu Chakwera kwa usimamizi mbaya na kutokuwa na maamuzi, na pia kushindwa kukabiliana na ufisadi na kutekeleza ahadi za kuunda nafasi za kazi.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Wakati wa muhula wake, gharama zilipanda katika taifa hilo linalotegemea kilimo, mfumuko wa bei ukifikia asilimia 33 huku bei ya mahindi ya chakula na mbolea ikiongezeka, suala lililokuwa kuu katika uchaguzi huo.

“Katika siku zilizosalia, nataka mjue kuwa nimejitolea kukabidhi madaraka kwa amani, ninajua kwamba wengi wenu mliounga mkono kampeni yangu ya kuchaguliwa tena mtasikitishwa.” Chakwera alisema

Taarifa ya Joseph Jira