Israel na Marekani zazidisha mashambulizi dhidi ya Iran

Israel na Marekani zazidisha mashambulizi dhidi ya Iran

Kwa siku ya tano mfululizo Jeshi la Israel kwa ushirikiano na Marekani, limefanya mashambulio mapya katika ardhi ya Iran dhidi ya kile imekitaja kuwa kuangamiza kabisa utawala wa kigaidi huku ikiionya Iran kujiandaa kwa mashambulio makubwa zaidi yatakayoisambaratisha miundombinu ya kijeshi ya nchi hiyo.

Mashambulio hayo ya usiku wa kuamkia leo Machi 4, yalilenga mji Tehran na Beirut, kama mwendelezo wa hujuma nzito za kijeshi baada ya lile shambulio la Februari 28, lililomuua kiongozi wa kidini Ayatola Ali Khameni.

Mwendelezo huo wa mashambilizi sasa yanaifikisha idadi ya watu waliouawa katika pande zote mbili takribani watu 700.

Mataifa kama vile Ufaransa, Urusi, na China yalitoa wito wa kusitishwa kwa haraka vita hivyo, lakini kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump haionyeshi dalili za kukomeshwa kwa mashambulio hayo baada ya kudokeza katika taarifa yake, kwamba vita hivyo huenda vikachukua zaidi ya wiki 5.

Kwa upande wake, Iran inazidisha mashambulizi yake dhidi ya taasisi muhimu za Israel na Marekani katika eneo la Mashariki ya kati na shambulio la hivi punde kabisa likilenga ubalozi wa Marekani huko Dubai na bandari Ya Fujairah.

Pia mashambulio hayo yanaendelezwa nchin Israel, ambako Idadi ya vifo vya Waisreali inazidi kuongezeka, ingawa hakuna taarifa kuhusu idadi kamili.

Viongozi wa juu wa Israel wamepiga marufuku kutangaza au kupiga picha mashambulizi yanayoyafanya ndani ya Israel.

Mashambilizi haya sasa yamesambaa katika eneo la Ghuba huku Mataifa ya kigeni yakianzisha mkakati wa kuwahamisha raia wao ambao wamekwama kufuatia kufungwa kwa anga za mataifa hayo.

Iran pia imefunga Mlango wa Bahari ya Hormuz ambayo ni muhimu kwa kupitisha takriban mapipa milioni 20 ya mafuta kila siku.

Hatua hii tayari imeathiri biashara ya kimataifa.

Taarifa ya Eric Ponda